1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasitisha usafirishaji wa mabomu kwenda Israel

8 Mei 2024

Marekani ilisitisha usafirishaji wa mabomu kwenda Israel wiki iliyopita baada ya serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kushughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu mpango wake wa kuuvamia mji wa Rafah.

https://p.dw.com/p/4fcFI
Mabomu yakipakiwa kwenye ndege ya kivita ya Marekani
Marekani imekuwa ikipinga operesheni ya ardhini ya Israel katika mji wa RafahPicha: Mike Nelson/dpa/picture alliance

Marekani ilisitisha usafirishaji wa mabomu kwenda Israel wiki iliyopita baada ya serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kushughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu mpango wake wa kuuvamia mji wa Rafah, ulioko kusini mwa Gaza.

Afisa mwandamizi katika utawala wa Rais Joe Biden, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, ameeleza kuwa Marekani ilizuia usafirishaji wa shehena ya mabomu kwenda Israel wiki iliyopita.

Afisa huyo ameongeza kuwa bado hawajafanya uamuzi kuhusu iwapo wataendelea na usafirishaji wa silaha hizo.

Utawala wa Biden ulifanya uamuzi wa kuzuia usafirishaji wa shehena hiyo ya silaha baada ya Israel kuonekana kuwa tayari kuendelea na oparesheni kubwa ya kijeshi mjini Rafah, operesheni ambayo imepingwa vikali na Marekani.