1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Marekani yapinga muswada wa UN wa kusitisha mapigano Gaza

Lilian Mtono
9 Desemba 2023

Marekani imetumia kura ya turufu kupinga muswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4ZxY2
Marekani, New York | Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Marekani ilipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lililenga kuhamasisha usitishwaji wa mapigano mara moja kati ya Israel na Hamas huko Gaza.Picha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Azimio hilo la Umoja wa Mataifa liliungwa mkono na wanachama 13 kati ya 15 wa Baraza hilo. Uingereza ambayo ni mwanachama mwingine wa kudumu wa Baraza la Usalama haikupiga kura.

Naibu Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Robert Wood amelikosoa baraza hilo baada ya kura hiyo, akisema limeshindwa kulilaani shambulizi la wanamgambo wa Hamas nchini Israel pamoja na kutambua haki ya Israel ya kujilinda. Ameongeza kuwa kusitisha mapigano kutatoa mwanya kwa Hamas kuendelea kulitawala eneo la Gaza na kufanya mashambulizi mengine ya kigaidi.

Wood, amesema, azimio hilo pia halikuzingatia uhalisia wa mambo na wala haliwezi kubadilisha chochote huko Gaza.

Marekani inalipinga azimio hili licha ya maonyo ya shirika la kimataifa linaloshughulikia afya, WHO kwamba hali inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Shirika hilo Christian Lindmeier amesema watu katika eneo hilo sasa wanakata milingoti ya nyaya za simu na kuwashia moto wa kuota ili angalau kujikinga na baridi na pengine kupikia, pale wanapokuwa na chochote cha kupika.

Marekani, New York | Maandamano nje ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Marekani, New York | Waandamanaji wakiwa nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakihudhuria mkutano wa kushughulikia mzozo wa kibinadamu katikati ya mzozo kati ya Israel na Hamas, mjini New York, Marekani, Disemba 8, 2023.Picha: David Dee Delgado/REUTERS

Guterres aonya dhidi ya 'adhabu ya pamoja' kwa Wapalestina

Kabla ya kikao hicho cha dharura, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ukatili unaofanywa na wanamgambo wa Hamas usitumike kuhalalisha adhabu ya pamoja kwa Wapalestina.

Guterres amesema hayo huku akitoa wito wa kuachiliwa mara moja mateka 130 ambao bado wanazuiwa na Hamas, tena bila ya masharti yoyote.

Aidha, amerudia tena kauli yake kwamba hakuna mahali salama katika Ukanda wa Gaza na raia wameshiwa chakula.

IDF: Wanajeshi wawili wajeruhiwa katika jaribio la kuokoa mateka 

Mzozo wa Mashariki ya Kati | Mashambulizi ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza
Picha hii iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) mnamo Desemba 3, 2023 inaonyesha wanajeshi wa Israel wakiendesha operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.Picha: IDF/Xinhua/picture alliance

Nchini Israel, jeshi la taifa hilo, IDF limesema jana Ijumaa kwamba wanajeshi wake wawili walijeruhiwa vibaya baada ya kujaribu kuwaokoa mateka wanaozuiwa Gaza. Limesema katika operesheni hiyo, watekaji wawili pia waliuawa na hakukuwa na mateka yoyote aliyeokolewa.

Hamas, ambao wanaorodhoshwa kama magaidi na Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine wamesema kwenye taarifa yao kwamba walifanikiwa kulizuia jaribio la Israel la kuwaokoa mateka wa Israel inaowashikilia. Bila ya kuthibitisha, wanamgambo hao wamesema mateka mmoja aliuawa wakati walipokabiliana na wanajeshi wa IDF. Israel haikazungumzia madai hayo.

Umoja wa Ulaya wawaongeza viongozi wa Hamas kwenye orodha ya ugaidi

Huku hayo yakiendelea, Umoja wa Ulaya jana Ijumaa umewaweka makamanda wawili wa Hamas katika orodha ya magaidi, kama sehemu ya kujibu kitisho kinacholetwa na kundi hilo pamoja na mashambulizi yake ya kigaidi nchini Israel, Oktoba 7, 2023. Makamanda hao ni mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas, Mohammed Deif na naibu wake Marwan Issa.

Baraza la Umoja huo limesema, fedha za viongozi hao wawili pamoja na mali nyingine za kifedha katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, zitazuiwa.

Soma pia:Mapigano makali yaendelea Ukanda wa Gaza